Lugha, mataifa tofauti lakini kinyago kimoja

22 Mar, 2013

HABARILEO
BY MAGNUS MAHENGE


UWANJA wa Karimjee Dar es Salaam, Tanzania umekutanisha wachonga vinyago zaidi ya 100 kutoka mabara mbalimbali kushindanisha na kuadhimisha Siku ya Miti Duniani ili kuchambua umuhimu wa miti.

Kitu cha kushangaza kwa wachongaji hao, wakiwa wamejipanga kuchonga vinyago kwenye makundi kadiri ya maeneo au nchi wanazotoka, wamewasiliana wao kwa wao katika makundi si na wengine, jambo ambalo halikuathiri uchongaji.

Waandaaji wa Siku ya Miti Duniani Machi 21, Howard Rosen kutoka Marekani, Victoria Amoros kutoka Ufaransa, Monlin Kuo kutoka Marekani, Su Jinling kutoka China, Mario Tomazello Filho kutoka Brazili na Yang Ping kutoka Japan, bila kujali umbali wa mabara watokayo, wamefanikisha kuwakutanisha wachongaji ambao hawajui lugha nyingine, isipokuwa za maeneo watokayo.

Wachonga vinyago wamekutana ili kushindanisha miti ya kwao inayotumika katika kuchonga vinyago, kwani kadiri ya jiografia duniani, kila eneo lina miti ya aina tofauti na lingine na uoto wake wa asili ni tofauti na mwingine.

 

Lakini pia, wamekutana katika kujadili na kujua historia ya miti na umuhimu wa kutumia miti hiyo kutoka mikoa na nchi tofauti, katika kuleta maendeleo ya mtumiaji na mazingira yake.

Bila kujali tofauti za lugha au mataifa wanayotoka, wamekutana kujadili kinaga ubaga maendeleo na utamaduni wa kutumia mazao ya miti, mfano samani, karatasi, vifaa vya nyumbani, mbao, marembo, mbao za kuandikia na za kuchonga vinyago.

Utumiaji wa miti katika kudumisha utamaduni wa miti katika makabila, mataifa na watu wa maeneo mbalimbali, lugha mbalimbali, wenye filosofia tofauti na sanaa za uchongaji anuwai.

Lakini pia wanafanya uhamasishaji wa matumizi ya miti katika jamii zote duniani na katika hatua zote za kutoa elimu ya miti duniani.

Wataalamu hao wenye taaluma ya miti na matumizi yake, wanahamasisha mtazamo chanya wa miti, matumizi yake, mfano katika kutengeneza na kudumisha uzuri wa miti, faida, uoto wa asili, mazingira yake na historia yake pamoja na matumizi miti katika kijamii.

Mkusanyiko huo wa wachonga vinyago, umefanyika bila kuathiriwa na lugha, utaifa wala umbali, bali unataka kutambulisha umuhimu wa miti.

Jambo muhimu kwao si lugha, wala kuwasiliana bali ni kuonesha ubora wa miti hata kama watumiaji hawana lugha moja, hawatoki bara moja wala si taifa moja.

Joseph Senya wa Mwenge Dar es Salaam, hafahamiani na Huachan Yang wa China, ambaye hata kadi yake ya biashara imeandikwa kichina, lakini wote wawili ni mahiri katika kuchonga vinyago, hivyo kwao ni sawa na 'kinyago kimoja mataifa na lugha tofauti.’

Wachina kutoka Mashariki ya Mbali hawajui Kiswahili cha Senya wa Mwenge, Dar es Salaam wala Kingereza cha Phyllius Hogan wa Kikundi cha Sanaa na Mitishamba cha Marekani, wanajua Kichina peke yake.

Yang wa China na Higan wa Marekani, ndio kwanza wameingia Tanzania iliyopo Afrika Mashariki, hawajui Kiswahili, lakini kwa kutumia miti ya kwao hawana wasiwasi wanapokuwa na wachonga vinyago wenzao wa Tanzania.

Michael Andoba wa Mtwara, Tanzania hakujua Kifiji anachozungumza Paula Ligairua, hata hivyo wote wawili walikuwa wakizungumza na wenzao kutoka Tanzania au Fiji, lakini waliendelea kuchonga kinyago bora kutokana na mti wa nchi zao.

Benjamin Ogunbamise kutoka Nigeria, alikuwa akichonga kinyago cha mshikamano kikubwa na kizuri, lakini alikuwa akizungumza lugha ya nyumbani kwao, Kihausa au Kiyoruba, wala hakijui Kiswahili wala Kiingereza cha India, Marekani na Uingereza.

Joseph Nunga wa Mtwara, anajua Kiingereza vizuri, lakini alishindwa kuwasiliana na Mchina, Jonah Hill wa kampuni ya Kuchonga Vinyago ya Hopi Wood, hata kama wabunifu hao walikuwa wakichonga na kutumia zana tofauti za uchongaji.

Mwandishi wa Makala haya, naye alipata wakati mgumu kuuliza majina ya Wachina, hata hawakujua kuonesha kadi zao za biashara, licha ya mwandishi kujitahidi kuonesha kadi nyingine, hawakujua anasema nini, lakini hiyo haikuwazuia kuendelea na kuchonga vinyago vya miti ya njano.

Menbere Shafi wa Sudan wakati mahojiano yakiendelea na Waswahili, yeye alikuwa bize akichonga sanamu ya umoja wa bibi na bwana, hakuwa anasikia Kiswahili, hakusumbuka kusikiliza, aliendelea kuchonga kinyago chake.

Rajabu Pili wa Burundi, hata kama yupo katika nchi mojawapo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, alikuwa na wakati mgumu kuzungumza Kiswahili, alimung’unya maneno, hata Kiingereza kilipita koshoto, aliongea Kirundi, lakini kazi ya sanaa ilifanyika bila shida.

Licha ya waandaaji kukusanya wachongaji kutoka Mashariki hadi Magharibi, Kusini na Kaskazini wasio zungumza lugha moja, lakini walijua wanaweleta pamoja wachongaji vinyago bila kujali lugha tofauti na mataifa yao.

Hivyo kinyago kilichochongwa kutokana na miti ya rangi na ubora tofauti duniani, kimeleta pamoja na kutengeneza umoja wa wachongaji vinyago duniani nchini Tanzania.

Maonesho, mashindano na maadhimisho yanayofanyika kwa mara ya kwanza nchini, yameungwanishwa kwa kinyago.

Uchongaji huo uliotanguliwa na kongamano la kujadili miti, faida na maendeleo yake, limehitaji wakalimani wengi wa kutafsiri lugha, hata kama wachongaji hawakuhitaji wakalimani wakati wa kuchonga vinyago.

Kongamano hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania, bara la Afrika, limekuwa likifanyika nchini China tangu 2006, katika miji tofauti Beijing, Jilin, Nanning, Changsha na mingine ambako wamekuwa wakitumia Kichina, lakini wamelileta Tanzania ambako Kiswahili kinatumika, lakini hakijakwamisha uchongaji.

Shughuli za kuonesha uchongaji vinyago, zilianza mwaka jana, katika nchi ya Benin, Cameroon, mwaka huu imefanyika Tanzania, lugha haijawa kikwazo.

Jamii inayodumisha Utamaduni wa Mbao ya Kimataifa, iliyoamua kuleta maonesho na maadhimisho ya Siku ya Miti Duniani Machi 21, Tanzania, wamefanya hivyo kuonesha kuwa miti ipo mahali pote duniani na matumizi yake pia, hayafungwi na lugha, mipaka wala jiografia.

Watanzania mahiri katika kuchonga vinyago kutoka mikoa mbalimbali nchini japo hawajui Kiingereza au Kichina, wameshiriki kikamilifu katika kuonesha vipaji vyao katika kushindana kuchonga wao kwa wao au na wengine.

Watanzania kama Adriano Mbano kutoka Ruvuma, Alphonce Kusalale kutoka Lindi, Augustione Mwiru kutoka Mtwara, Constantine Albino kutoka Ruvuma na George Lugwani kutoka Pwani wamewakilisha uchongaji vinyago kwa kutumia mti aina ya mninga, japo hawajui lugha za kigeni.

Hakuna upinzani kwamba lugha ni kiunganisho bora katika mawasiliano, lakini kuna vitu vingine kama sanaa, alama za ishara hta michezo kama mpira wa miguu zinaweza kutumika kuwasiliana.

Maonesho ya uchongaji vinyago kutumia miti mahalia, ni miongoni mwa vitu vilivyowaunganisha watu katika kuwasilisha na kuonesha taaluma kwa umma.

Kumbe inawezekana mataifa mbalimbali kufanya kazi pamoja na kuishi pamoja, ama wakatumia alama lakini pia wakatumia bidhaa wanazotengeneza kama kazi ya kuchonga kinyago iliyowakutanisha watu bila kuwa na lugha moja.

Other Related Posts


World Wood Day