Bidhaa za miti zaineemesha Tanzania

22 Mar, 2013

HABARILEO
BY MAGNUS MAHENGE


RASILIMALI zitokanazo na misitu ni muhimu na ndio maana ukawepo msemo huu, 'misitu ni uhai', yaani bila misitu hakuna uhai.

Misitu ikikosekana hakuna kiumbe kitakachoishi kiwe cha majini, nchi kavu na angani na popote pale duniani. Binadamu na viumbe wengine wenye pumzi, wanahitaji rasilimali za misitu kwa matumizi mengi, tiba zote, kuni na mbao, miti ya kujengea, nyumba za binadamu na ndege na hata mvua inanyesha kutokana na kuwepo misitu.

Kwa kutambua umuhimu wa misitu, Shirika la Kimataifa la Utamaduni wa Kutunza Misitu (IWCS), kwa kushirikiana na mashirika mengine mengi ya duniani wameandaa maonesho ya bidhaa za miti.

Mashirika hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na nyingine zinazohusiana na hiyo, wameamua kuandaa na kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani Machi 21 (jana), kwa kufanya maonesho na mashindano ya bidhaa za miti.

Siku ya Misitu Duniani mwaka huu imeadhimishwa, jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kwa kuwakutanisha wachongaji vinyago na wasanii maarufu kutoka pande zote za dunia.

 

Wachonga vinyago kutoka Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi mwa dunia, wamefika jijini Dar es Salaam kuonesha umahiri wa uchongaji wao na kushindana na wachonga vinyago wengine na kuitambulisha miti maarufu katika uchongaji vinyago hivyo.

Uwanja wa Karimjee, Dar es Salaam, ulifurika wachonga vinyago, wabunifu na wasanii mahiri wa sanaa za asili, wakionesha uhodari wao katika kutengeneza zana zitokanazo na miti na kushindana katika kutengeneza vinyago vya mitindo mbalimbali.

Lakini pia maadhimisho hayo, yameamsha ari ya kutambua umuhimu wa miti kwa ajili ya watu wa kawaida pamoja na viwanda, kwani miti ni mshiriki mkubwa wa maendeleo ya binadamu na uendelezaji mazingira.

Pamoja na kuonesha rasilimali hiyo, kutakuwa na mashindano ya kuchonga vinyago kutokana na miti maarufu duniani na mshindi atapata nafasi ya kushiriki katika mashindano mengine duniani.

Mchongaji mahiri kutoka Visiwa vya Fiji, Paula Liga, anasema amefurahi kufika Tanzania, lakini kubwa ni kuona namna Waafrika wanavyochonga vinyago kwa kutumia zana za zamani, lakini nzuri.

Liga anasema mitindo ya uchongaji imepishana na ina tofauti kubwa na huko kwao, hata hivyo wasanii wote wanatumia rasilimali za miti. Mchongaji vinyago wa Kitanzania, Focus Senya anasema ameshikwa na kigugumizi kuona tofauti kubwa ya uchongaji vinyago baina ya Waafrika na Wazungu.

“Wenzetu wameendelea kwa kutumia vifaa vya kisasa na sisi bado tunatumia zana za zamani, na nyingine zinatokana na miti yenyewe,” anasema. Mashindano hayo yalitanguliwa na kongamano la kujadili umuhimu na matumizi ya miti duniani. Katika kongamano hilo, watafiti na wachunguzi wa miti wa kimataifa, wametoa au kueleza uchunguzi wao kuhusu miti ya Afrika inavyotumika katika kuleta maendeleo.

Lakini pia wameonesha namna miti ilivyo msaada na namna inavyochangia kuleta utamaduni tofauti, lakini pia wamejadili kuhusu matumizi ya kihistoria ya miti na malengo endelevu ya kutunza miti.

Uchongaji wa vinyago umefanyika uwanjani, ambapo wachongaji kutoka katika nchi mbalimbali duniani wanaonesha taaluma yao ya kuchonga kwa kutumia zana au vifaa anuwai vya kisasa na vya zamani.

Wachongaji kutoka Tanzania, hasa kutoka Mtwara, Kagera na Dar es Salaam eneo la Mwenge, wamejitokeza kushiriki katika mashindano hayo ya kutambulisha umahiri katika uchongaji vinyago.

Watanzania wanashindana kwa uchongaji na wengine kutoka katika nchi nyingine barani Afrika, jambo ambalo limeonesha tofauti kubwa ya taaluma ya uchongaji.

Watu binafsi, vikundi na vyama mbalimbali vya uchongaji vimejitokeza ama kwa lugha nyingine, Tanzania imejitokeza kujipima kiuchongaji na mataifa yaliyobobea katika fani hiyo, na hivyo imepata changamoto ya viwango vyao.

Katika kuhitimisha uchongaji huo, kumekuwa na mashindano ya uchongaji vinyago ambapo nchi zote zilizoshiriki kutoka katika mabara ya Ulaya, Amerika Kusini, Kaskazini, Asia, Afrika na Australia zimeshirikisha wachongaji wake kujua nani bingwa wa fani hiyo.

Lucy Maina, mmoja kati ya Watanzania waliofika kuona mashindano hayo ya uchongaji amesifia ukuaji wa taaluma hiyo na matumizi ya zana za kisasa, tofauti na zamani. Mashindano ya kuangalia umuhimu wa miti katika sanaa ni ya kwanza kufanyika Tanzania, Afrika na duniani, lakini yameibua changamoto nyingi, ambazo bila Shirika la IWCS kuandaa mashindano hayo, zisingebainika.

Mashindano hayo yameibua vipaji vya watoto wenye taaluma ya kuchora vinyago na katuni za miti. Kadhalika, mashindano na maonesho ya vifaa vinavyotokana na na miti, hasa vinyago, yametumika katika kuonesha umuhimu wa kulinda, kudumisha na kuendeleza mazingira.

Kutokana na umuhimu huo, wachongaji wa nje pamoja na Watanzania watashiriki katika kupanda miti mingine ili uchongaji usiwe unaharibu miti bali uwe endelevu kwa kupanda miti mingine ili kutumiwa na kizazi kijacho.

Wachongaji waliofika katika kuonesha vinyago vyao, watakuwa na nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali yakiwamo ya Zanzibar kuona matumizi ya miti mbalimbali duniani.

Miti kwa wakati wa sasa, imekuwa chimbuko la sanaa, pia inaleta furaha hasa kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha tiba na afya, lakini pia inadumisha utamaduni wa makabila na mataifa mbalimbali. Lakini pia miti inachangia kuweka kumbukumbu za vitu mbalimbali, picha, matukio ya viongozi na imekuwa chimbuko la kuweka rekodi mbalimbali.

Katika kuhitimisha maonesho wachongaji, ubunifu na uchongaji huo, hasa kuhusu mashindano hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki ametoa zawadi na tuzo kwa wote walioibuka washindi katika maonesho na mashindano hayo ya aina yake nchini na Afrika kwa ujumla.

Other Related Posts


World Wood Day